ELIMU YA KODI KWA MJASIRIAMALI NI MUHIMU SANA. WENGI HUIKWEPA KAMA TUNAVYOKWEPA ELIMU YA AFYA.



ELIMU YA KODI KWA MJASIRIAMALI NI MUHIMU SANA. WENGI HUIKWEPA KAMA TUNAVYOKWEPA ELIMU YA AFYA.

Kuna kodi kadhaa zinazomhusu mjasiriamali mdogo kwa ngazi ya taifa na ngazi za halmashauri. Kuna kodi ya mapato ambayo mjasiriamali ni mlipaji wa moja kwa moja kutoka kwenye biashara yake.

Kuna tozo za manispaa kama tozo ya huduma (service levy) nazo pia hutoka moja kwa moja kwenye biashara ya mjasiriamali. Ila zipo kodi ambazo hazitoki moja kwa moja kwa mjasiriamali ila yeye anapaswa kuwasilisha TRA baada ya kuzikisanya. Mfano wa kodi hizi ni kama VAT na kodi ya zuio (withholding tax).

KODI YA ZUIO (WITHHOLDING TAXES) NI KAMA
1. Malipo ya pango.... Mfano umepanga frem ama ofisi ya biashara yako na malipo ya pango unatakiwa ulipe 500,000 kwa mwezi. Unachopaswa kufanya ni kumlipa mwenye frem ama ofisi 450,000 na 50,000 iliyobaki utaiwasilisha TRA ndani ya siku saba za mwezi unaofata. Kila malipo ya kupanga ofisi au frem kumbuka unapaswa kulipa asilimia 90 kwa mwenye nyumba na asilimia 10 TRA. Usipofanya hivyo ukibainika TRA watakukadiria na kukutoza wewe uliyepanga na wana haki ya kukupiga penati na riba.

2. Mathalan umemlipa mtaalam kwa kukushauri ama kukuandalia mchanganuo ama kukusaidia kuajiri na kadhalika. Malipo unayomlipa inapaswa kuwa asilimia 95 ya kiasi mlichokubaliana. Mfano kama amesema gharama yake ni 200,000 yeye atapata 190,000 na 10,000 iliyobaki utaiwasilisha TRA ndani ya siki saba za mwezi unaofata.
Hizo mbili ndio zinawagusa watu wengi sana japo kuna kodi nyingi nyengine za zuio.

KODI YA MAPATO
Kwa kawaida kodi ya mapato hupatikana kutokana na faida ya mjasiriamali. Iwapo mjasiriamali ni mtu binafsi basi atalipa kodi kulingana na jedwali la kodi la watu binafsi na iwapo ni kampuni basi atalipa kodi ya mapato ya makampuni ambayo ni asilimia 30 ya faida inayokokotolewa kwa kufuata sheria za kodi ya mapato.

Kuna nyakati ambazo kodi ya mjasiriamali ambae ni mtu binafsi atahesabiwa kodi kutoka katika mauzo kama ifuatavyo:
1. Mauzo kwa mwaka hayazidi 4,000,000. Hatozwi kodi ya mapato.

2. Mauzo kwa mwaka 4,000,000-7,500,000 na ana kumbukumbu za mahesabu => kwa mwaka atatozwa 3% ya mauzo yote yanayozidi 4,000,000. Kama hatunzi kumbukumbu basi kwa mwaka atatozwa 150,000.

3. Mauzo kwa mwaka 7,500,000-11,500,000 na ana kumbukumbu za mahesabu => kwa mwaka atatozwa 135,000 jumlisha 3.8% ya mauzo yote yanayozidi 7,500,000. Kama hatunzi kumbukumbu basi kwa mwaka atatozwa 318,000.

4. Mauzo kwa mwaka 11,500,000-16,0500,000 na ana kumbukumbu za mahesabu => kwa mwaka atatozwa 285,000 jumlisha 4.5% ya mauzo yote yanayozidi 11,500,000. Kama hatunzi kumbukumbu basi kwa mwaka atatozwa 546,000.

5. Mauzo kwa mwaka 16,000,000-20,000,000 na ana kumbukumbu za mahesabu => kwa mwaka atatozwa 487,000 jumlisha 5.3% ya mauzo yote yanayozidi 16,000,000. Kama hatunzi kumbukumbu basi kwa mwaka atatozwa 862,000.

6. Mauzo kwa mwaka zaidi ya 20,000,000 mjasiriamali anapaswa kufunga mahesabu kila mwaka na yakaguliwe na mkaguzi wa mahesabu.

7. Mauzo zaidi ya 14,000,000 kwa mwaka lazima mjasiriamali atumie mashine ya kodi ya EFD. Asipotumia TRA wana haki ya kumtoza faini kati ya 3,000,000 na 4,500,000.
Mfanyabiashara huyo pia atalipishwa pia mara mbili ya kodi ambayo alipaswa kuitoza kwa bidhaa aliyouza ama kufungwa kwa kifungo kisichozidi maika mitatu ama vyote kifungo na mara mbili ya kodi alopaswa kuitoza kwenye bidhaa aliyoiuza.

8. Mauzo chini ya 14,000,000 lazima yatolewe kwenye kitabu cha risiti cha kuandika kwa mkono na kopi za risiti zitunzwe. Risiti lazima ionyeshe tarehe, jina la biashara yako, TIN namba yako, bidhaa ama huduma iliyouzwa, thamani ya pesa, na jina na makazi ya mnunuzi.
Kumbuka kuwa hizo kodi zinamhusu kila mtu binafsi ambae anafanya biashara iwe ni bishara ya kununua na kuuza duka ama rejareja, iwe ya kutoa ushauri, awe anatoa huduma kama mwanasheria, wakili, ama msaidizi wa masuala ya kisheria, iwe ni fundi ujenzi, fundi umeme, fundi bomba na kadhalika. 
Kodi ni mada ndefu na nitaendelea kadiri ninavyojaaliwa. 

Comments

Popular Posts